Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Mauaji Yanayotekelezwa na Polisi: Akili ya Kibepari Iliyojaa Ukatili na Kutoadhibiwa
(Imetafsiriwa)
Maafisa watatu wa polisi nchini Kenya wameshtakiwa kwa kumuua mwanablogu mwenye umri wa miaka 31, ambaye alifariki akiwa kizuizini polisi mapema mwezi huu. Kifo cha Albert Ojuang kimezua hasira nchini Kenya, ambako maandamano yameandaliwa kutaka haki itendeke.
Tunapenda katika Hizb ut-Tahrir / Kenya kuangazia yafuatayo:
Vyombo vya usalama chini ya mfumo wowote wa kidunia wa kiliberali, kama vile Kenya, ni muendelezo wa mfumo wa kikoloni uliotumiwa na Waingereza kuwatawala watu na kukandamiza upinzani. Katika miaka ya hamsini, Wakenya walipoanza kudai haki yao ya kujitawala, polisi na vyombo vingine vya usalama vya Uingereza viliwakamata makumi elfu yao na zaidi ya elfu walinyongwa. Inaonekana kuwa vikosi vya polisi vinawaona watu wa kawaida kama tishio linalowezekana kwa utawala, mbinu ambayo hapo awali iliwekwa ili kutekeleza utawala wa kikoloni, na sio kuwalinda.
Kihakika, mifumo ya kidunia ya kiliberali hutukuza maslahi na manufaa kuliko maisha na mali za binadamu, na kufanya rushwa, kutoadhibiwa na unyakuzi wa dola kuwa sheria ya kisiasa. Kwa kuzingatia hili, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola bila kuadhibiwa ndiyo njia pekee ya kukandamiza sauti yoyote ya upinzani au juhudi za kufichua rushwa kubwa. Ikumbukwe kwamba ukatili na mateso yanayofanywa na vyombo vya dola ni mwelekeo wa kimataifa na si kwa Kenya pekee.
Tunasisitiza kwamba maisha ya binadamu, au tuseme roho zote, ni takatifu na zinastahili ulinzi kamili kutoka kwa dola bila hofu au upendeleo. Katika Uislamu, kulinda maisha ya binadamu ni muhimu sana, na kunachukuliwa kuwa amana takatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uislamu unasisitiza utakatifu wa nafsi, na unakataza kuichukua bila haki, na unaamrisha kuhifadhiwa na heshima yake kwa wanadamu wote.
Tunasisitiza kwamba chini ya Khilafah Rashidah kwa njia ya Utume itakayosimamishwa karibuni, kwa idhini ya Mungu, vikosi vya polisi vitakuwa na jukumu la kudumisha utulivu wa umma, kutekeleza sheria na kuchunguza uhalifu. Mateso yameharamishwa kabisa, na afisa yeyote wa polisi atakayepatikana na hatia ya kufanya shambulio la mwili au mateso dhidi ya mtu yeyote, awe Muislamu au si Muislamu, atawajibishwa. Kwa hivyo, vikosi vya polisi vitajikita kikamilifu katika kudumisha sheria na utulivu na hivyo kulinda maisha na mali za raia.
Shabaan Mwalimu
Mwakilishi wa Habari wa Hizb ut-Tahrir
Kenya