Uanaharakati - Mwelekeo Mpya wa Syria
(Imetafsiriwa)
Habari:
Mnamo Agosti 25, 2025, Rais wa Syria, Ahmed al-Shara, alitangaza wakati wa mkutano na ujumbe wa ngazi ya juu wa vyombo vya habari vya Kiarabu, kwamba hajioni kama muendelezo wa vyama au harakati zozote za Kiislamu, iwe za kijihadi, au za Udugu wa Kiislamu, au hata za Arabu Spring. Kulingana na Nadim Qutaish, Mkurugenzi Mkuu wa Sky News Arabia, al-Shara pia alifichua kuwa kuna mazungumzo ya ngazi ya juu yanaendelea kuhusu makubaliano ya kiusalama na taasisi ya Kizayuni, kwa msaada wa Marekani na nchi za Ghuba. Huku akikiri kwamba mazingira bado hayajawa sawa kwa ajili ya kufikia mkataba kamili wa amani, al-Shara alisema kuwa hatasita kutafuta makubaliano kama hayo ikiwa yatahudumia "maslahi" ya Syria. (Syrian Observer).
Maoni:
Kujitenga kwa Ahmed al-Shara kutoka kwa makundi ya Kiislamu haishangazi kwa kuzingatia mkondo wake wa kuachana na mtazamo wa kutawala kwa Uislamu, na kuwapa wafuasi wa Bashar al-Assad kinga chini ya kauli mbiu ya "Maridhiano ya Kitaifa", na sasa kushiriki katika mazungumzo na taasisi ya Kiyahudi. Hatua hizi zinaonyesha kwamba urithi wake wa kisiasa sio wa Uislamu au Arabu Spring, lakini wa utamaduni wa kitaifa wa kilimwengu ambao kwa muda mrefu umetawala tabaka tawala nchini Syria.
Kinyume chake, watu wa Syria na mapinduzi yao yaliyobarikiwa wameeleza mara kwa mara utambulisho wao na matarajio yao ya Kiislamu. Slogani zao zilijumuisha imani na dhamira: "Ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, si kwa ajili ya mamlaka wala umaarufu", na "Ee Mwenyezi Mungu, hatuna mwingine ila Wewe, Ee Mwenyezi Mungu" na "Khilafa milele, licha yako, Ee Assad". Wakati watu walijumuisha uaminifu, kujitolea na ubora, matamko na matendo ya Ahmed al-Shara yalidhihirisha uanaharakati wa kisiasa, makubaliano na kupuuza maono ya Kiislamu ya mapinduzi.
Inasikitisha sana kuona mapinduzi ambayo yametoa dhabihu kubwa - familia, riziki na maisha yaliyotolewa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na hukumu yake - yakitwaliwa na utawala ambao sasa unatafuta uhalali kwa idhini ya Amerika na taasisi ya Kiyahudi. Hizi ndizo nguvu zile zile ambazo zinashiriki katika uharibifu wa Syria na mauaji ya kimbari yanayoendelea ya umma wetu huko Gaza. Maneno ya Mtume ﷺ yanasikika kwa nguvu katika muktadha huu: «Yeyote anayetafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa hasira ya watu, Mwenyezi Mungu atamridhia na atawafurahisha watu kumhusu, na yeyote anayetafuta radhi za watu kwa hasira ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamkasirikia na atawakasirisha watu kumhusu».
Kama wafuasi wa Mtume wetu mpendwa ﷺ, Waislamu hawakatai tamaa kamwe. Vita vya Handaki ni ukumbusho wa milele: Wakati Maquraishi na washirika wao walipoizingira Madina, ulimwengu ulikuwa mgumu kwa Waislamu kutokana na njaa na shida, lakini katika msiba huo, Mtume ﷺ alitangaza ushindi; funguo za Sham, Uajemi na Yemen. Historia hii inatufundisha kwamba hata katikati ya dhoruba, waumini hubaki imara na wenye matumaini, wakitambua kwamba misiba hupita na kwamba ushindi wa Mwenyezi Mungu unakuja bila shaka.
Basi wajibu wa Umma ni kuendelea kujenga msukumo kuelekea ushindi wa lazima kwa kuungana kuzunguka Uislamu na kukataa makubaliano ambayo hudhoofisha kanuni zetu. Ukombozi wa kweli wa Syria na nchi zote za Kiislamu utapatikana tu kwa kuanzisha Khilafa iliyoongoka kwa mfumo wa Utume, mfumo ambao unahakikisha haki, uwajibikaji na heshima kwa Umma.
Imeandikwa kwa ajili ya Radio ya Ofisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir
Muhammad Al-Shami