Suluhisho la Mataifa Mawili Ni Suluhisho la Kikoloni kwa Suala la Palestina
(Imetafsiriwa)
Habari:
Wakati Gaza inaendelea kuwaka moto, na makumi ya watu wake wanauawa kila siku, kwa mabomu na njaa, na vurugu zinaongezeka katika Ukingo wa Magharibi mikononi mwa uvamizi wa kinyama, msukumo umefanywa upya, haswa kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi, kuelekea suluhisho la mataifa mawili, ambalo wanadai litatayarisha njia ya kutatua mzozo unaoendelea kwa miongo kadhaa katika eneo hilo. Ufaransa, Uingereza na Kanada, miongoni mwa nchi zingine, zimetangaza nia yao ya kuitambua dola la Palestina, ikiwa masharti maalum yatatimizwa. Vile vile, mkutano mkuu wa kimataifa uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Julai, ulioongozwa na Ufaransa na Saudi Arabia, ulijadili umuhimu wa kuweka hatua madhubuti za kufikia suluhisho la mataifa mawili. Mkutano huo ulitoa tangazo la kurasa saba linalounga mkono lengo hili, ambalo pia liliungwa mkono na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Ulaya.
Maoni:
Suluhisho la mataifa mawili kwa suala la Palestina ni suluhisho la kikoloni la Kimarekani, ambalo huibuka kila mara ambapo mataifa mbalimbali ya kikoloni yanajaribu kugeuza usikivu wa kimataifa kutoka kwa jukumu wanalolichukua katika kuunga mkono na kuimarisha chombo cha Kiyahudi chenye kiu ya damu, na kujionyesha kama watengeneza amani, jambo ambalo liko mbali sana na ukweli. Katika hali hii, wito wa nguvu za kikoloni kutambua dola la Palestina ni pazia la moshi tu la kujaribu kugeuza usikivu kutoka kwa hasira za ndani na za kimataifa juu ya ushiriki wao unaoendelea katika mauaji haya ya kimbari ya watu wa Gaza, kwa kukipatia chombo hicho silaha. Ni mchezo wa kuigiza wa kidiplomasia ambao haubadilishi chochote katika hali halisi!
Serikali hizi za kikoloni zinatambua vizuri kwamba utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili, ambapo inadhaniwa dola la Palestina litaishi kwa amani kando ya dola la Kiyahudi, ni wazo la kubuni lisilowezekana kabisa, na limetenganishwa na ukweli. Kwa kweli, imekuwa mzaha ulio wazi kati ya duru zao za kidiplomasia, ambao wanatambua kuwa hakuna njia ya kuunda dola kutoka Ukingo wa Magharibi na mashariki mwa Jerusalem ambayo inajumuisha makazi zaidi ya 200 na karibu walowezi 700,000, ambayo imetenganishwa na Ukanda wa Gaza na ardhi inayokaliwa ambayo imeteketezwa kabisa na uvamizi. Walakini, wanaendelea kupeperusha wazo la suluhisho la mataifa mawili kana kwamba ni fimbo ya uchawi ambayo inaweza kufuta miongo kadhaa ya dhuluma, unyakuzi wa ardhi, mauaji ya halaiki, kufungwa, na utakaso wa kikabila wa watu wa Palestina na Wayahudi!
Zaidi ya hayo, wito wa suluhisho la mataifa mawili hautakomesha uhalifu unaoendelea wa chombo cha Kiyahudi dhidi ya watu wa Palestina au kukomesha lengo lake la upanuzi la kuunda "Israeli Kubwa" na kunyakua ardhi yote iliyobarikiwa. Hii ndiyo njia iliyo wazi ya sera ya chombo cha Kiyahudi. Kwa kweli, serikali ya Kiyahudi inajadili mipango ya kujenga maelfu ya nyumba mpya katika eneo la E1, mashariki mwa Jerusalem Mashariki, ambayo itaunganisha makazi makubwa ya Ma'ale Adumim na Jerusalem. Hii itasababisha kuibiwa kwa takriban ekari 3,000 ili kujenga nyumba zaidi ya 4,000 za makazi, ambayo itagawanya na kutawanya Ukingo wa Magharibi na kuutenga zaidi. Netanyahu pia ametangaza mipango ya kukalia Ukanda wa Gaza.
Kwa hivyo ni wazi kuwa suluhisho la mataifa mawili ni ndoto tupu! Rabie Eghbariah, wakili wa haki za binadamu, anaandika: "Ukweli ni kwamba suluhisho la mataifa mawili limekuwa udanganyifu; kauli mbiu inayorudiwa kuficha ukweli wa dola moja iliyoimarishwa. Kutoka Mto Yordani hadi Bahari ya Mediterania, 'Israeli' inadhibiti maisha ya watu wote wa Palestina, bila haki sawa, bila uwakilishi sawa, na kwa mfumo uliojengwa kudumisha ubora wa Kiyahudi."
Zaidi ya hayo, dola la Palestina litakuwaje? Litakuwa dola lisilo na mamlaka halisi, lisilo na ardhi iliyo na muunganiko, lisilo na manufaa ya kiuchumi, lisilo na udhibiti wa mipaka yake, maji, na anga, na lisilo na jeshi la kulilinda dhidi ya maadui zake, lililozungukwa na chombo cha uvamizi cha uhalifu ambacho kimethibitisha kwa ulimwengu kuwa hakijali sheria au makubaliano yoyote ya kimataifa, au viwango vya kimaadili, au uhuru wa nchi! Kwa maneno mengine, litakuwa dola lisilo na maana! Ongeza kwa hayo kwamba kukubali suluhisho la mataifa mawili kunamaanisha kukubali dola la Palestina kwenye 20% au chini ya ardhi iliyobarikiwa. Hii inamaanisha kukubali wizi wa chombo cha Kiyahudi cha ardhi ya Palestina, kukubali utakaso wake wa kikabila, na uhamaji wa halaiki wa watu wa Palestina kutoka makwao, matumizi yake ya ugaidi, mauaji, kukamatwa, na ubomoaji wa nyumba ili kupanua mamlaka yake juu ya ardhi, na kukubali haki ya uvamizi wa uhalifu wa kuwepo kwa kutambua mipaka yake ya kudumu. Hili linawezaje kuwa la haki au la kimaadili au sahihi?! Kwa hivyo, suluhisho la mataifa mawili ni njia ya kejeli tu inayotumiwa na nguvu za kikoloni kuwalazimisha Waislamu kukubali uwepo wa chombo cha Kiyahudi, na kuacha ardhi ya Waislamu iliyokaliwa, na kupuuza miongo kadhaa ya uhalifu mbaya wa uvamizi!
Kukubali chini ya ukombozi kamili wa Palestina ni usaliti kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ﷺ na dini yetu. Pia kunapaswa kuwepo dola linalounganisha ardhi iliyobarikiwa na nchi zingine za Waislamu, na kutawala kwa sharia ya Mungu na mfumo wake. Dola hili ni Khilafah Rashidah ya Pili kulingana na mfumo wa Utume; ni yenyewe tu inayoweza kufikia haki, kuhifadhi haki na heshima ya raia wake wote bila kujali dini yao, na kuanzisha amani na usalama kwa wote chini ya utawala wake, kama ilivyofanya kwa karne nyingi. Kwa hivyo, tukiwa Waislamu, lazima tukatae udanganyifu wowote wa kikoloni, na tuitikie wito wa kuanzisha dola la Khilafah kulingana na mfumo wa Utume, ambalo litakomesha mauaji haya ya kimbari, na kuwatendea haki watu wa Palestina, na kukomboa ardhi yetu yote!
﴿Enyi mlio amini! Itikieni wito wa Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuwaiteni kwenye lile linalo kuhuisha.﴾
Imeandikwa kwa ajili ya idhaa ya Ofisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir
Asmaa Sediq
Mwanachama wa Ofisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir