Kwa Waziri wa Awqaf wa Morocco: Hudumia Dini Wala Usiitumie, Ukaonyesha Batili Katika Sura ya Haki!
Habari:
Waziri wa Awqaf na Masuala ya Kiislamu wa Morocco, Ahmed Al-Tawfiq, ameanzisha tena mjadala kuhusu mapato ya benki na dhana ya riba, wakati wa ushiriki wake katika kongamano la uthabiti wa kifedha ya Kiislamu, lililoandaliwa na Benki ya Morocco na Baraza la Huduma za Kifedha za Kiislamu Alhamisi 2025/07/03 katika mji mkuu Rabat. Alisisitiza kuwa shughuli za kifedha na mapato ya mikopo zinahusiana na "sheria" yaani, mkataba na ridhaa ambayo inahakikisha uadilifu, zaidi ya inavyohusiana na "ibada", akieleza kuwa uadilifu unahitaji kwamba ulazima usigeuke kuwa fursa ya dhuluma na uonevu kwa mkopaji, na hili linahitaji uingiliaji kati wa uongozi kulinda pesa kwa sheria na taasisi. (Gazeti la Elaph)
Maoni:
Hii haikuwa kauli ya kwanza ya Waziri wa Awqaf wa Morocco kuhusu kuhalalisha riba, bali ilitanguliwa na usomaji wake wa kisasa wa shughuli za benki alizoshiriki mwaka jana katika somo la Hassani la Ramadhani alilotoa mbele ya Mfalme Muhammad VI, ambapo alikosoa "baadhi ya wazungumzaji wa dini ambao waliaibisha dhamiri za Waislamu kwa kusema kwamba riba ni faida ya mkopo kwa faida yoyote ile", na akaeleza kuwa "mikopo mingi katika enzi hii ni kwa sababu ya ulazima au uwekezaji, na kile kinacholipwa kwa faida kinahusiana na bei ya muda na malipo ya huduma", wakati "faida inapungua kadiri uchumi unavyokua nchini". Anaona kwamba hekima ya Qur'ani Tukufu katika kuharamisha riba ilikuja kukata uhusiano na mazoea ambayo yalikuwa yameenea katika baadhi ya ustaarabu wa kale, ambapo mazoea haya yalikuwa yakitegemea kumtumikisha mtu asiyeweza kulipa deni kwa mapato mara dufu, jambo ambalo baadhi ya wanafalsafa wa Ugiriki walilikemea.
Waziri huyu wa Awqaf ambaye anavisha haki kwa batili na anawasihi watu kuwa na uhakika kwamba shughuli za kawaida za benki haziko nje ya Uislamu mradi tu ziko ndani ya mfumo wa mkataba na haziko mara dufu, na kwa hivyo anaona kwamba anatimiza maslahi ya umma kwa kufanya upya hotuba ya kidini na kuondoa pengo kati ya "uelewa wa kisheria usiobadilika" na hali halisi ya maisha ya Waislamu, bali anapigana na maandishi ya kisheria ya uhakika, thabiti katika Kitabu na Sunnah na Ijma, na kwa hivyo uharamu wa riba haukubali tafsiri au ubadilishaji na mapato bila kujali kiasi chake bali huingia katika riba.
Imam Al-Ghazali anasema: "Ama maslahi ni usemi asili yake ni kuleta manufaa au kuondoa madhara; na hatumaanishi hivyo; kwa sababu kuleta manufaa au kuondoa madhara ni makusudio ya viumbe; na wema wa viumbe uko katika kupata makusudio yao, lakini tunamaanisha kwa maslahi: kuhifadhi kusudi la sheria" (Al-Mustasfa: 1/217).
Kila kheri kwa waja inapatikana kwa kumtii Allah Mtukufu, na kwa hivyo maslahi yanatimizwa, na kuridhiana hakuhalalishi kile ambacho Allah amekiharamisha, na Imam Al-Shatibi ameeleza kuwa radhi ya wahusika haiondoi uharibifu uliokusudiwa na katazo la kisheria, lakini kuridhiana kunazingatiwa kwa sababu inaonyesha hamu ya pande zote mbili na hakuna kulazimishwa kwao, sio kwa sababu inachochea uhalali wa mkataba. Kwa hivyo, mapato yaliyokubaliwa kwa ridhaa ya pande zote mbili, hata ikiwa ni kidogo, hayaondoi kutoka kwa mkataba tabia yake ya riba. Basi ni vyema kwa Waziri wa Awqaf kutochezea hukumu za kisheria na kutumia vibaya wadhifa wake katika kutumia dini badala ya kuuhudumia, kupotosha watu na kuwaficha kwamba serikali imechukua roho ya sheria na kufuata makusudio yake kwa kuwarahisishia watu! Kuhusu hili, Imam Ibn Qayyim al-Jawziyya anasema: "Basi ni kweli kwa yule anayemcha Mungu na kuogopa adhabu yake kuogopa kuhalalisha yale ambayo Mungu ameyaharamisha kwa aina za hila na udanganyifu, na ajue kwamba hakuna kinachomwokoa kutoka kwa Mungu kile anachoonyesha kwa hila na udanganyifu wa maneno na matendo, na ajue kwamba Mungu ana siku ambayo siri zinafichuliwa, na kile kilicho ndani ya vifua kinapatikana, huko wanajua wadanganyifu kwamba walikuwa wanajidanganya wenyewe, na walikuwa wanacheza na dini yao, na hawafanyi hila isipokuwa kwa nafsi zao na hawatambui" (I'lam al-Muwaqqi'in (3/163) kwa ufupi).
Ushauri wetu kwa Waziri wa Awqaf ni kwamba asiwalazimishe watu kubeba dhambi zao na akumbuke kauli yake Mwenyezi Mungu: ﴿Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa katika Moto, watasema: Laiti tungemtii Mwenyezi Mungu na tungemtii Mtume. Na watasema: Mola wetu! Hakika sisi tuliwatii viongozi wetu na wakubwa wetu, basi wakatupoteza njia. Mola wetu! Wape adhabu mara mbili na uwalaani laana kubwa﴾.
Imeandikwa kwa ajili ya Radio ya Afisi ya Habari Kuu ya Hizb ut-Tahrir
M. Durra Al-Bakoush