2025-11-05
Jarida la Ar-Raya: Mtego wa Ukraine na mustakabali wa NATO
Mipango ya kivita ya kuizunguka Urusi na kuizingira China
Jumuiya ya kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) imeanza kuweka mipango ya kivita na tafiti za siku za usoni kuhusu vita kati yake na Urusi, na nchi za NATO zimepitisha na kuandaa "maelfu ya kurasa za mipango ya kijeshi" ambayo ilielezewa kuwa "ya siri", na zinazohusiana na makabiliano yanayowezekana na Moscow. Mipango hii inajumuisha maelezo ya makabiliano ya kijeshi yanayowezekana na Urusi kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, na wataalamu wanasema: "Hii ni kwa sababu NATO, baada ya kuanza kwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, ilikagua sera yake kuelekea Shirikisho la Urusi, ambalo haikuliona kwa muda mrefu kama tishio kubwa kwa muungano."
Mwanzoni, Urusi ilijaribu kujiunga na NATO na kufanya makubaliano nayo, ambapo ilisaini nayo mwaka 1997 Sheria ya Msingi ya Uhusiano kati yao, ambayo inawalazimu kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani, demokrasia na usalama. Kulikuwa na kizuizi cha kuwekwa kwa nguvu za mapigano za ziada za NATO katika nchi za muungano, lakini iliruhusiwa katika kesi ya kujilinda na ikiwa kuna tishio. Pia walikubaliana juu ya ushirikiano wa kisiasa wa muda mrefu na Baraza la NATO na Urusi liliundwa kama jukwaa la ushauri wa pamoja.
Lakini kukataa kwa nchi za NATO kujiunga na Urusi, na kisha kufuata sera ya "mlango wazi" na kupanua kuelekea mashariki, kulifanya Urusi kuhisi kusalitiwa na kudhalilika baada ya kuzungumza juu ya hakikisho la siri lililotolewa kwa viongozi wa Magharibi la kutokupanua kuelekea mashariki na kutojumuisha Ukraine. Lakini nchi za Magharibi ziliwadanganya, kama Putin alivyosema katika hotuba yake ya kutangaza vita dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022: "Mlituahidi katika miaka ya tisini kwamba NATO haitasonga inchi moja kuelekea mashariki. Mmetudanganya kwa ujasiri. Mawimbi matano ya upanuzi wa NATO (yametokea) hadi sasa."
Mnamo tarehe kumi na nane ya mwezi wa Mei 2022, Finland na Sweden ziliwasilisha ombi rasmi la kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), na kuachana na sera ya kutopendelea upande wowote ambayo wamefuata kwa miongo kadhaa.
Marekani iliona kuangusha Urusi kwenye mtego wa Ukraine kama mafanikio ya malengo makuu, kwa sababu vita vya Urusi na Ukraine havikuanza kiasili, lakini vilitengenezwa na Marekani kwa malengo makuu ya kimkakati, kupitia kuingia kwa Urusi kwenye vita baada ya mazungumzo kuhusu kujiunga kwa Ukraine na NATO, na kuongeza muda wake hadi malengo yanayotakiwa yafikiwe.
(Makadirio ya kijeshi karibu na Kremlin yalionyesha kuwa operesheni ya kijeshi haitachukua zaidi ya siku chache kukamilisha kazi iliyokabidhiwa, ambayo inahusiana na kuunganisha baadhi ya majimbo ya Ukraine na Urusi. Lakini utawala wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden ulikuwa na maoni tofauti, kwani ilipata malengo yake ya kijiografia katika vita vinavyoendelea mashariki mwa Ukraine, kwa hivyo haikusita kufungua madaraja ya msaada wa kijeshi, kijasusi na vifaa kwa Kyiv ili kuzuia shambulio la Urusi) (Al Jazeera)
James Landale, mwandishi wa masuala ya kidiplomasia katika Shirika la Utangazaji la Uingereza, aliandika kuhusu hili: "Labda malengo ya vita dhidi ya Urusi ndiyo chanzo muhimu zaidi cha mvutano. Hivi sasa, nchi za Magharibi zimeungana nyuma ya kauli mbiu ya kutetea Ukraine, na zinatoa msaada wa kiuchumi na kijeshi kusaidia nchi hiyo kupinga, lakini lengo ni nini kwa muda mrefu?"
Jarida la Kimarekani la The National Interest lilisema: "Kwamba Marekani imepitisha mbinu ya busara katika vita vya Ukraine, kwa kuweka majeshi yake mbali na mapigano ya moja kwa moja, na kuchagua kuunga mkono Kyiv kama nguvu mbadala ndani ya mkakati mpana unaolenga kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa kawaida wa Urusi, bila kuhatarisha maisha ya askari wa Marekani au kuhusika katika mzozo wa moja kwa moja kati ya NATO na Urusi."
CJ Atkins, mhariri mkuu wa jarida la World People, anaashiria katika makala yake kuhusu mtego wa Ukraine, kwamba unyonyaji wa wasiwasi halali wa kiusalama wa Urusi, pamoja na matarajio ya kifalme ya serikali ya Putin, ulifanya kuweka mtego kuwa wa moja kwa moja, ikiwa si rahisi. (Al-Araby Al-Jadeed)
Na Putin, kama kawaida ya Warusi wanaojulikana kwa upungufu na ujinga wa kisiasa, alianguka kwenye mtego na kudhani kwamba vita vya Ukraine havitatumia muda mrefu, na ukweli ni kwamba Ukraine ilikuwa chambo ambayo dubu wa Urusi aliimeza bila kutambua sifa za sera ya Marekani na malengo yake.
Marekani inalenga kufikia malengo matatu kutoka kwa vita vya Ukraine, ambayo ni:
1. Kuimaliza nguvu Urusi na si kuimaliza kabisa. Maafisa wakuu wa Magharibi walieleza hilo waziwazi; wakiongozwa na Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, ambaye alisema kuwa "lengo ni kuona Urusi katika hali dhaifu". Ndiyo, Urusi ilianguka kwenye mtego na kudhani kwamba Ukraine ingeanguka ndani ya siku chache na kwamba msaada wa Magharibi ungetoweka. "Lakini mbinu hii iligongana na hali tofauti, badala ya kuanguka, safu ya Ukraine iliungana na iliungwa mkono na uhamasishaji wa umma na utangazaji wa kimataifa, ambao ulishindwa shambulio la haraka, na kulazimisha vikosi vya Urusi kurudi nyuma, na kugeuza mzozo kuwa vita vya muda mrefu vya kuimaliza nguvu."
2. Kuitisha Urusi na kuzitisha nchi za Ulaya ili zibaki chini ya ulinzi wa Marekani na zisifikirie kujenga mfumo wa ulinzi wake yenyewe. Biden amefanikiwa kuonyesha Urusi kama tishio kubwa kwa nchi za Magharibi, na kwa hivyo majaribio hayo ya kujenga uhusiano endelevu wa Ulaya na Urusi yalitoweka, kwa sababu ya mgongano wa maono ya kimkakati kati ya pande hizo mbili. Jarida la The National Interest liliripoti kuwa vita vya Urusi vilichangia kufufua NATO, ambayo ilishuhudia uchovu katika miongo iliyofuata Vita Baridi. Hii ilisababisha kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi ya washirika wa Ulaya, na kujiunga kwa nchi zilizokuwa hazipendelei upande wowote kama vile Sweden na Finland na muungano huo, ambao uliimarisha mshikamano wake na jukumu lake la usalama katika bara la Ulaya, lakini muungano huo uliongeza bajeti yake ya kiraia kwa 27.8% kufikia zaidi ya euro milioni 370 na kuongeza bajeti yake ya kijeshi kwa 25.8% kufikia karibu euro bilioni 2. Hatimaye, vita vilionyesha kwamba Ulaya bado inahitaji mwavuli wa usalama wa Washington na kuzuia migogoro ya Ulaya na Ulaya na uongozi wake wa muungano.
3. Kuvunja uhusiano kati ya Urusi na China, bali kujaribu kuijumuisha Urusi baada ya kuizunguka ili iwe sehemu ya mkakati wa kuizingira China. Kudhoofisha Urusi na kuimaliza nguvu zake katika vita ni kudhoofisha China pia, jambo ambalo Marekani inafaidika nalo. Kwa sababu ya vita nchini Ukraine, China inaweza kupoteza mshirika muhimu ambaye alikuwa anaiunga mkono kimataifa na kuratibu nayo misimamo ya kidiplomasia, na kwa hivyo makadirio mabaya ya Putin katika vita yalisababisha kuishirikisha China naye, kwa kiasi fulani, katika kinamasi cha Ukraine.
Jarida liliendelea: "Kwa hivyo Washington ilikuza faida yake kutokana na imani hii katika kipindi cha hivi karibuni na ilifanya kazi ya kuongeza kasi ya uratibu wa kijeshi na kubadilishana uzoefu kati ya wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) huko Uropa na washirika wake katika Asia Mashariki kama vile Japan, Korea Kusini na Australia, na uratibu huu wa kimkakati unasababisha upanuzi wa ushawishi wa Washington na kuongezeka kwa uwezo wake wa kukabiliana na Moscow na Beijing."
Kwa hivyo, Marekani haitaki kuimaliza Urusi kwa kisingizio cha upanuzi wa wigo wa vita na hofu ya vita vya nyuklia, kwa hivyo iliendelea kuiunga mkono Ukraine kwa uangalifu, lakini haikuipatia silaha hatari na za kukera, kwa hivyo misaada ilikuwa kwa kiwango fulani kufikia malengo ya vita.
Kutokana na kuongezeka kwa muda wa vita, mwelekeo wa Ulaya na Marekani ulitofautiana, lakini Ulaya haina uamuzi hata kuhusu usalama wake, wala kuhusu vita vya Ukraine, lakini siyo mmiliki wa uamuzi wa kisiasa kwa sababu mazungumzo ni kati ya Urusi na Marekani. Ulaya inataka kusimamisha vita bila masharti ya awali kwa sababu inachomwa na moto wake na athari zake na matokeo yake. Na Urusi, ambayo imepoteza heshima yake na kupoteza zaidi ya robo milioni ya wapiganaji kulingana na takwimu za Magharibi, inamfuata Trump ili kufanya mkutano ili kuhifadhi heshima yake, na Trump anajizuia, jaribio lake la kufikia lengo la tatu kuhusiana na kuizingira China.
Gazeti la Telegraph la Uingereza lilichapisha uchambuzi wenye kichwa: "Hadithi ya nguvu ya Putin inaanguka .. Labda mwisho uko karibu kuliko anavyofikiria," iliyoandikwa na Mark Brulin, mtaalamu wa masuala ya kimkakati ya kijiografia, ambaye alidai kuwa hadithi ya nguvu ya Rais wa Urusi Vladimir Putin ilianza kuporomoka, na kwamba mwisho wa utawala wake unaweza kuwa karibu kuliko wengi wanavyofikiria, na wa kwanza wao ni Putin mwenyewe, akizingatia kwamba mabadiliko ya hivi karibuni katika msimamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuelekea Moscow yanaweza kuharakisha mwisho wa vita nchini Ukraine na labda kuanguka kwa utawala wa Urusi wenyewe.
Imeandikwa na: Profesa Hassan Hamdan
Chanzo: Jarida la Ar-Raya