Mpango wa Musaiki: Marekebisho ya Mkakati Uliofeli na Jaribio Jipya la Kuwadhibiti Taliban
(Imetafsiriwa)
Habari:
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni lilifanya kikao maalum kujadili hali nchini Afghanistan. Katika kikao hicho, Rosa Otunbayeva, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi nchini Afghanistan (UNAMA), aliwasilisha mfumo mpya mpana unaoitwa "Mpango wa Musaiki". Alisisitiza kuwa mpango huu haulengi "kuhalalisha hali nchini Afghanistan", bali unalenga kukuza maslahi ya kweli ya watu wa Afghanistan.
Maoni:
Ufunuo wa mpango mpya unakuja baada ya kushindwa kwa mpango wa awali wa Umoja wa Mataifa, uliowekwa na Feridun Sinirlioğlu. Juhudi hizo zilifikia mwisho mbaya katika pande kuu mbili: kwanza, ukosefu wa makubaliano ya kimataifa juu ya jinsi ya kushughulika na Taliban; na pili, kukataa kwa Taliban mjumbe maalum aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa, ambaye alikuwa na jukumu la kutekeleza mpango huo. Kwa kuzingatia vikwazo hivi, Umoja wa Mataifa umezindua mpango mpya unaoitwa "Musaiki".
Ili kutekeleza mkakati uliopita, mikutano ya Doha ilifanyika, na iliendelea kwa raundi tatu. Hata hivyo, kama ilivyoelezwa hapo awali, mchakato ulikwama kutokana na changamoto zilizotajwa hapo juu. Sasa, baada ya mwaka mmoja, mchakato wa Doha umeanza tena. Mnamo Juni 30 na Julai 1, 2025, Qatar iliandaa mkutano wa tatu wa Kamati ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na mkutano wa pili wa kiufundi kati ya Taliban na wawakilishi wa sekta binafsi ya kimataifa. Mikutano hii miwili ilifanyika kama sehemu ya awamu ya nne ya mchakato wa Doha na ndani ya mfumo wa utekelezaji wa mpango wa Musaiki. Ingawa mkutano wa mwisho ulikuwa wa kiufundi kwa asili, unaonekana sana kama utangulizi wa mazungumzo ya kisiasa ya baadaye. Kulingana na taarifa iliyotolewa mnamo Mei 2, 2025 na Stephan Smith, msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi nchini Afghanistan, mpango wa Musaiki unatokana na nguzo mbili muhimu:
- Kuanzisha vikundi vya kazi ili kukabiliana na changamoto za dharura zinazowakabili watu wa Afghanistan, kama vile juhudi za kupambana na dawa za kulevya na kukuza sekta binafsi.
- Kushughulikia vikwazo vya msingi vinavyozuia Afghanistan kurudi katika mfumo wa kimataifa, hasa ahadi ya haki za binadamu na kuheshimu sheria za kimataifa.
Licha ya Musaiki kuwasilishwa kama mpango mpya, kimsingi ni toleo lililorekebishwa la mpango uliopita. Malengo ya kimkakati hayajabadilika, isipokuwa marekebisho ya mbinu za utekelezaji na ushiriki. Kama Rosa Otunbayeva alivyoeleza wakati wa kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama kuhusu Afghanistan: "Ushiriki wa maana na Afghanistan unalenga kujenga taifa linaloishi kwa amani na lenyewe na na majirani zake, linatii majukumu yake ya kimataifa, na linarudi katika ushirikiano katika jamii ya kimataifa - sio taifa linalobaki limekwama katika mzunguko wa vurugu unaorudiwa".
Taarifa hii inaonyesha wazi kuwa lengo kuu la mpango bado ni kutenganisha taratibu Taliban kutoka kwa mtazamo wao wa Kiislamu, na hatimaye kuunganishwa katika mfumo wa kidunia wa kimataifa.
Moja ya sifa bainifu za mpango wa Musaiki ni mkakati wake wa hatua kwa hatua. Katika mfumo huu, ikiwa Taliban itachukua hatua kuelekea mfumo wa kimataifa, Magharibi itajibu kwa hatua kama hiyo. Sera hii inategemea udhibiti wa taratibu na ushawishi unaosimamiwa. Hata hivyo, Taliban imeshindwa hadi sasa kuwasilisha mpango wazi na madhubuti wa kutumia utawala wa Kiislamu au mfumo kamili wa kisiasa wa Kiislamu. Ulimwengu wa Magharibi umetumia fursa hii, na kuwalazimisha Taliban kukubali mfumo wao wenyewe. Kwa upande mwingine, Hizb ut-Tahrir, chama cha msingi na cha kisiasa cha Kiislamu, kinatoa maono kamili, halali na ya kweli ya kuanzisha Khilafah Rashidah, mradi ambao unategemea kabisa kanuni za Kiislamu. Tofauti na mbinu ya taratibu ya Magharibi, mpango huu sio wa taratibu, lakini unategemea msingi wa Uislamu. Kulingana na Uislamu, wakati mwingine nia njema pekee inatosha kwa Mwenyezi Mungu kurahisisha na kufungua njia. Na nyakati zingine, ikiwa mja atachukua hatua moja, Mungu humkaribia hatua, kama ilivyo katika Hadith Qudsi: «Ikiwa mja hunikaribia shubiri, mimi humkaribia dhiraa, na ikiwa mja hunikaribia dhiraa, mimi humkaribia baa, na ikiwa ananijia kwa kutembea, mimi humjia kwa kukimbia» Imesimuliwa na Bukhari na Muslim
Imeandikwa kwa ajili ya idhaa ya Ofisi ya Habari Kuu ya Hizb ut-Tahrir
Yusuf Arsalan
Mjumbe wa Ofisi ya Habari ya Hizb ut-Tahrir katika jimbo la Afghanistan