Silaha ya "Uchukizo dhidi ya Wayahudi" Kunyamazisha Uungaji Mkono Ukombozi wa Palestina
(Imetafsiriwa)
Habari:
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mjadala mkubwa nchini Uingereza ambao unaonyesha kuwepo kwa uhusiano kati ya maandamano ya kuunga mkono Palestina na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi na mashambulizi dhidi ya Wayahudi nchini humo. Kabla ya kumbukumbu ya pili ya shambulio la Hamas dhidi ya taasisi ya Kiyahudi mnamo Oktoba 7, 2023, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliwahimiza wanafunzi wasijiunge na maandamano ya kuunga mkono Palestina siku hiyo, akionya juu ya "kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi katika mitaa yetu," na kwamba "si jambo la Kiingereza kutowaheshimu wengine" kwa kuandaa maandamano katika kumbukumbu hii, akiongeza kuwa maandamano hayo yametumiwa na wengine "kama kisingizio duni cha kuwashambulia Wayahudi wa Uingereza." Msemaji wake alisema kuwa waandamanaji "wanapaswa kuonyesha ubinadamu wao" na kukumbuka shambulio dhidi ya taasisi ya Kiyahudi mnamo Oktoba 7, wakati Waziri wa Elimu, Bridget Phillipson, pia aliwasihi watu wasifanye maandamano katika kumbukumbu hii, akisema: "Miaka miwili baada ya Oktoba 7, ningependa tu kuwaomba watu watafakari na kujaribu kufikiria ubinadamu wetu wa pamoja na wajibu wetu kwa kila mmoja." Baadhi pia walilaumu maandamano ya kuunga mkono Palestina nchini humo kwa shambulio dhidi ya sinagogi la Manchester mnamo Oktoba 2, ambalo lilisababisha vifo vya wanaume wawili Wayahudi.
Maoni:
Ni wazi kwamba serikali ya Uingereza, na idadi ya wanasiasa wengine, na wachambuzi wa vyombo vya habari wanaounga mkono taasisi ya Kiyahudi, wanatumia karata ya chuki dhidi ya Wayahudi kujaribu kunyamazisha wito wa ukombozi wa Palestina kutoka kwa Wayahudi. Waziri wa Mambo ya Ndani, Shabana Mahmood, pia ametangaza mipango ya kuwapa polisi mamlaka pana ya kuzuia maandamano ya mara kwa mara, kufuatia maandamano mengi ya kuunga mkono Palestina, wakati Waziri wa Afya, Wes Streeting, anakusudia kusasisha sheria zinazowazuia madaktari na wafanyikazi wengine wa afya wanaochukia Wayahudi kuwatibu wagonjwa. Wengi katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Magharibi wanaona chuki dhidi ya Wayahudi kama wito wa kuondoa kabisa uvamizi kutoka Palestina. Kwa hivyo, wafanyikazi wa afya wanaoonyesha uungaji mkono wao kwa ukombozi kamili wa Palestina wanakabiliwa na hatari ya kupoteza kazi zao chini ya kivuli cha chuki dhidi ya Wayahudi.
Simulizi inayoenezwa ambayo inaunganisha chuki dhidi ya Wayahudi na wito wa kukomesha uvamizi wa kikatili na kuunga mkono haki ya Wapalestina kurejesha ardhi yao na nyumba zao ambazo zimeporwa kikatili na walowezi, ni simulizi ya kipuuzi kabisa, na pia kuchanganya matendo ya watu binafsi wanaowashambulia Wayahudi nchini Uingereza na maandamano ya kuunga mkono Palestina. Ni sawa na kulaumu maandamano ya kuunga mkono Ukraine kwa mashambulizi dhidi ya watu wa Urusi nchini Uingereza. Ni simulizi inayotumiwa waziwazi kuwatisha na kuwanyamazisha wale wanaodai kukomesha uvamizi huu wa kikatili na ukombozi kamili wa Palestina.
Zaidi ya hayo, dhana kwamba maandamano katika kumbukumbu ya pili ya Oktoba 7 juu ya mauaji ya halaiki huko Gaza, wakati uvamizi unaendelea kuwashambulia kwa mabomu Wapalestina wasio na hatia, ni jambo lisilo na hisia au linaonyesha ukosefu wa ubinadamu wa pamoja, linaonyesha viwango viwili vya wanasiasa wa Magharibi kuelekea thamani ya maisha ya Wapalestina ikilinganishwa na maisha ya Wayahudi wanaoishi ndani ya taasisi hiyo. Sio wito wa ukombozi kamili wa Palestina ndio unaochochea chuki dhidi ya Wayahudi katika nchi za Magharibi, lakini mauaji haya ya halaiki yanayofanywa na taasisi ya Kiyahudi, ambayo wanasiasa na vikosi vyake vinakubali dhana ya Kizayuni ya ubora wa Kiyahudi, na wanatumia Uyahudi kuhalalisha matendo yao ya kikatili na uvamizi wa ardhi takatifu. Zaidi ya hayo, sio Uislamu ambao una historia ya chuki dhidi ya Wayahudi ya kimfumo na uonevu wa Wayahudi, lakini ni nchi za Ulaya za kilimwengu. Kwa kweli, uanzishwaji wa taasisi ya Kiyahudi yenyewe ni matokeo ya mauaji ya Wayahudi huko Uropa, na hisia za chuki dhidi ya Wayahudi ndani ya Uingereza ambayo ilijaribu kuzuia mtiririko wa Wayahudi wa Ulaya kuingia nchini kupitia Sheria ya Wageni ya 1905.
Kinyume chake, Wayahudi walistawi chini ya dola ya Ukhalifa. Kwa mfano, mwanahistoria Myahudi wa Uingereza, Cecil Roth, anasema kwamba matibabu mema ambayo Wayahudi walipata katika Ukhalifa wa Ottoman yaliwavutia kutoka kote Ulaya, na ardhi ya Uislamu ikawa ardhi ya fursa kwao, ambapo walistawi kiuchumi. Chini ya Ukhalifa, Wayahudi waliokolewa na kupewa mahali salama walipodhulumiwa katika nchi zingine. Kwa mfano, mnamo 1492, Sultan Bayezid II alituma jeshi lake lote la majini kuokoa Wayahudi 150,000 wa Uropa ambao walikuwa wanadhulumiwa na watawala Wakristo wa Uhispania, na akawaweka katika ardhi za Ukhalifa. Zaidi ya hayo, mwanahistoria Myahudi Avi Shlaim alisema kwamba chuki dhidi ya Wayahudi ilihamishiwa kwa Waarabu kutoka Uropa, akisema kwamba chuki dhidi ya Wayahudi asilia ilikuwa karibu haipo katika eneo la Kiarabu kabla ya karne ya ishirini, na kwamba ilikuwa ni lazima fasihi ya Ulaya ya chuki dhidi ya Wayahudi itafsiriwe kwa Kiarabu ili eneo hilo lije kujua. Pia alisisitiza kwamba Wayahudi walijiunga vizuri katika jamii za Kiarabu kwa karne nyingi chini ya utawala wa Kiislamu, na kwamba aina ya kisasa ya chuki dhidi ya Wayahudi ni "ugonjwa wa Uropa" ambao umehamishiwa Mashariki ya Kati.
Kwa hivyo, Waislamu katika nchi za Magharibi wanapaswa kusimama imara mbele ya simulizi hizi za uongo na sera za serikali za vitisho zinazolenga kuwanyamazisha juu ya wito wa ukombozi kamili wa Palestina. Lazima tuendelee kutoa wito wa kung'oa uvamizi huu wa kikatili na mwuaji kutoka ardhi yote takatifu, kwani hili ndilo Mwenyezi Mungu anatuamrisha, na ndiyo njia pekee ya kukomesha mauaji na utumwa unaoendelea wa umma wetu huko. Tunapaswa kuchukua msukumo kutoka kwa matendo ya ndugu na dada zetu wapendwa huko Palestina ambao wametuonyesha ujasiri na ustahimilivu mbele ya dhuluma, inayotokana na imani yetu kama Waislamu. Hakika Mwenyezi Mungu Anasema: ﴿Hakika wale wanaosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakasimama imara, Malaika huwashukia wakawaambia: Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa﴾. Na lazima tuwaeleze wale walio karibu nasi kwamba mfumo wa Kiislamu unaotekelezwa na dola ya Ukhalifa kwa njia ya Utume ndiyo pekee inayoweza kupata amani, usalama, haki na ustawi na kuhakikisha haki za dini zote chini ya utawala wake huko Palestina na katika nchi zote za Kiislamu kama ilivyofanya katika historia.
Imeandikwa kwa Radio ya Afisi ya Habari Kuu ya Hizb ut Tahrir
Asmaa Sadiq
Mwanachama wa Afisi ya Habari Kuu ya Hizb ut Tahrir