Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye Utukufu Wote
(Imetafsiriwa)
Habari:
Siku ya Alhamisi, Baraza la Seneti lilipitisha kwa kauli moja azimio la kulaani tukio la kuuawa kwa wanandoa wawili mchana kweupe kwa amri ya baraza la jirga kwa jina la kile kinachoitwa "uhalifu wa heshima" huko Balochistan. Azimio hilo lilisema kuwa uhalifu huu wa kinyama hauwezi wala haupaswi kufichwa chini ya kisingizio chochote cha kiutamaduni, kikabila au kimapokeo, kwa kisingizio cha kile kinachoitwa "wivu" au "heshima". Kwa hakika ni uhalifu ambao umeudhalilisha sana heshima ya taifa. Jaribio lolote la kuhalalisha uhalifu huu kwa msingi wa "desturi au heshima" limekataliwa kabisa, kama ilivyo kwa mchakato mzima wa kulaumu mhasiriwa.
Maoni:
Hivi majuzi, video ya kutisha ya mauaji imesambaa sana kwenye mtandao, na kuchochea wimbi la hasira na mjadala wa umma. Tukio hili, ambalo liliripotiwa kutokea siku tatu kabla ya Eid al-Adha ya mwaka 2025 mwezi Mei, linaonyesha mwanamke akiongozwa hadi mahali pa jangwa na kupigwa risasi, kwa madai ya kufanya uhalifu ambao huenda alifanya au hakufanya. Video ilipokuwa ikipata nguvu, ilizua msisimko mkubwa wa vyombo vya habari, huku idadi kubwa ya watu wakitoa maoni. Jambo lililo wazi zaidi ni kwamba huu ni mauaji yaliyotekelezwa kwa jina la heshima; jambo ambalo linapotosha na kutumia vibaya maana ya neno hilo kwa njia ya kusikitisha.
Balochistan ndiyo mkoa mkubwa zaidi na tajiri zaidi wa rasilimali nchini Pakistan, mara nyingi huangaziwa kwa sababu za kusikitisha. Milipuko, utekaji nyara na tuhuma za uhaini ni masimulizi ya mara kwa mara yanayohusiana nayo. Hata hivyo, nyuma ya vichwa hivi vya habari kuna hali ya dhiki ya kimfumo. Licha ya kuwepo kwa taasisi za serikali - kutoka urasimu hadi mahakama - utawala wa sheria bado haupatikani kwa wengi. Mahakama Kuu ya Balochistan, inayoongozwa na jaji mkuu, ni sehemu ya mfumo mpana wa mahakama wa Pakistani, na imeundwa kutoa haki katika eneo hilo. Lakini kwa hakika, mahakama hii mara nyingi imewaangusha watu wanaopaswa kuwasaidia, na hivyo watu wamepoteza imani yao katika mfumo wa mahakama. Familia nyingi bado zinaomba majibu, zikitafuta wapendwa wao ambao wamepotea bila maelezo au baadaye kupatikana wakiwa wamekufa kando ya barabara. Miito hii ya kutaka haki ambayo haijatendeka inaonyesha jinsi mfumo ulivyo dhaifu na usivyofaa.
Chini ya utawala wa Khanate ya Kalat, Balochistan ilisimamiwa kulingana na masharti ya Sheria ya Kiislamu, ingawa ilikuwa imewekewa vikwazo fulani. Maqadhi (mahakimu Waislamu) walisimamia masuala ya kimahakama, huku maeneo ya kikabila yakiwa chini ya mamlaka ya Masardar, ambao, kwa mwongozo wa Maqadhi na mabaraza, walitekeleza haki iliyokita mizizi katika Sheria na desturi za kienyeji (Al-Rawaj). Hivyo, muda mrefu kabla ya utawala wa kikoloni, mifumo ya haki za ndani ilikuwepo katika eneo hilo. Jirga - pia inajulikana kama baraza, shura au panchayat katika maeneo mengine - ilitumiwa kutatua matatizo kupitia majadiliano na makubaliano ya jamii. Viongozi kama vile Sultan Bahlul Lodi na Sher Shah Suri waliunga mkono mila hizi na walishiriki katika mabaraza haya kutatua migogoro. Pamoja na kuwasili kwa Waingereza, kiini cha miundo hii ya jadi kilibadilishwa kwa ajili ya udhibiti wa kikoloni. Waingereza walianzisha mabaraza ya jirga, na kuwateua wakuu wa vijiji na viongozi wa kikabila kuwa mahakimu katika kesi za uhalifu mdogo, migogoro ya ndoa, uzinzi, na migogoro ya ardhi au mifugo. Wanachama hawa walichaguliwa na kusajiliwa na wakala wa kisiasa, na uamuzi wowote unaozidi miaka saba ulihitaji idhini ya wakala kwa gavana mkuu katika masuala mazito zaidi - hasa yale yanayohusiana na uaminifu kwa Uingereza - uamuzi ulitolewa na Shah Jirga, baraza kubwa la Masardar wakuu. Hivyo, mfumo ambao hapo awali uliundwa kufikia maelewano ya kijamii, ulibadilika hatua kwa hatua, na kufanya maamuzi yakichochewa zaidi na hisia, kulipiza kisasi na upendeleo wa kitamaduni. Dhana ya heshima tukufu (wivu) ilitumiwa kama silaha, na kugeuzwa kuwa uhalali wa vitendo vya unyanyasaji ambavyo havifanani na haki ambayo mifumo hii ilipaswa kuunga mkono. Kukemea kutoka kwa maafisa kunaonyesha kwamba inapingana na katiba ya Pakistan, lakini sababu ya kweli ya tatizo ni katiba isiyo ya Kiislamu na ukosefu wa utekelezaji wa Uislamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Surah Fatir: ﴿Yeyote anayetaka utukufu, basi utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu﴾.
Heshima pekee inayostahili kuuliwa au kuua kwa ajili yake ni sheria ya Mwenyezi Mungu. Katiba ya dola ya Khilafah itajumuisha mfumo wa kimahakama ambao utaundwa kulingana na Qur'ani na Sunnah, na wasimamizi wake hawatakuwa watumwa wa matamanio yao. Kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume ni njia pekee ya kulinda umma wa Mtume ﷺ dhidi ya dhuluma au kufanya uasi. Khalifa wa kwanza Rashid Abu Bakr Al-Siddiq alisema: "Mnyonge miongoni mwenu ni mwenye nguvu kwangu mpaka nimrudishie haki yake akipenda Mwenyezi Mungu, na mwenye nguvu miongoni mwenu ni mnyonge kwangu mpaka nimpokee haki yake akipenda Mwenyezi Mungu." Imesimuliwa na Al-Tabari na Ibn Hisham.
Imeandikwa kwa ajili ya Idhaa ya Ofisi Kuu ya Habari ya Hizb ut-Tahrir
Ikhlaq Jahan