Tafakari Katika Kitabu: "Miongoni mwa Misingi ya Saikolojia ya Kiislamu"
Kipindi cha Kumi na Moja
Himdi ni ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu, na sala na salamu zimwendee Imamu wa wacha Mungu, na Bwana wa Mitume, aliyetumwa kuwa Rehema kwa walimwengu, Bwana wetu Muhammad na kwa Aali zake na Masahaba zake wote, na utufanye pamoja nao, na utuhusishe katika kundi lao kwa Rehema Yako, Ee Mwingi wa Rehema kuliko wote wenye kurehemu.
Wasikilizaji wangu wapenzi, wasikilizaji wa redio ya Ofisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir:
Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh, na baada ya hayo: Katika kipindi hichi tunaendelea na tafakari zetu katika kitabu: "Miongoni mwa Misingi ya Saikolojia ya Kiislamu". Na kwa ajili ya kujenga haiba ya Kiislamu, pamoja na kuangalia akili ya Kiislamu na saikolojia ya Kiislamu, tunasema na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu:
Mwenyezi Mungu amesema katika Kitabu chake kitukufu, naye ndiye bora wa wasemaji: {Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}. (Aal Imran 31)
Al-Azhari amesema: "Kumpenda mja Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunamaanisha kumtii Yeye na wao, na kufuata amri zao". Na Al-Baydhawi amesema: "Upendo ni kutaka utiifu". Na Ibn Arafa amesema: "Upendo, kwa Waarabu, ni kutaka kitu kwa kusudi". Na Al-Zajjaj amesema: "Na kumpenda mtu Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni kumtii Yeye na wao, na kuridhika na yale ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha, na yaliyoletwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie. Na Mwenyezi Mungu amrehemu mshairi aliposema:
Unamuasi Mungu huku unadai kumpenda Hili haliwezekani katika kipimo, ni baya
Lau upendo wako ungekuwa wa kweli ungemtii Hakika mpenzi kwa anayempenda humtii
Na kumpenda Mwenyezi Mungu mja kunamaanisha msamaha, radhi, na thawabu, Al-Baydhawi amesema: "Mwenyezi Mungu atakupendeni: Atakusameheni, yaani atawaridhia". Na Al-Azhari amesema: "Na kumpenda Mwenyezi Mungu waja ni kuwaneemesha kwa msamaha", Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri}. (Aal Imran 32) Yaani hawawasamehi. Na Sufyan bin Uyayna amesema: "Mwenyezi Mungu atakupendeni" yaani atawakaribisha, na upendo ni ukaribu, na Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri, hawakaribishi makafiri". Na Al-Baghawi amesema: "Na kumpenda Mwenyezi Mungu waumini ni kuwasifu, na kuwathawabisha, na kuwasamehe". Na Al-Zajjaj amesema: "Na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, ni kuwasamehe, na kuwaneemesha kwa rehema Yake, msamaha Wake, na sifa nzuri kwao".
Enyi Waislamu:
Kinachotuhusu hapa ni kumpenda mja Mwenyezi Mungu na Mtume wake, upendo huu kwa maana iliyotajwa ni lazima, kwani upendo ni mwelekeo miongoni mwa mielekeo ambayo huunda saikolojia ya mwanadamu, na mielekeo hii inaweza kuwa ya kimaumbile, ya asili, haina uhusiano wowote na dhana yoyote, kama vile mwelekeo wa mwanadamu wa kumiliki, na kupenda kuishi, na kupenda haki, na kupenda familia na watoto..., na inaweza kuwa motisha inayohusiana na dhana, na dhana hizi ndizo zinazoamua aina ya mwelekeo, Wahindi wekundu hawakuwapenda wahamiaji kutoka Ulaya, wakati Ansar walikuwa wanawapenda wale waliowahama, na kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni aina ambayo Mwenyezi Mungu ameifunga kwa dhana ya kisheria ambayo ameifanya kuwa ni lazima, na dalili za hilo kutoka katika Kitabu:
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na katika watu wapo wanao wafanya badala ya Mwenyezi Mungu washirika, wanawapenda kama wanavyo mpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi}. (Al-Baqara 165) Na maana yake ni kwamba wale walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi kuliko mapenzi ya washirikina kwa washirika.
Na kauli yake: {Sema: Ikiwa baba zenu, na watoto wenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo chuma, na biashara mnayo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, vinakupendezeni zaidi kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu}. (At-Tawba 24)
Ama dalili kutoka katika Sunna, enyi Waislamu:
Ni nyingi, tunataja miongoni mwa hizo: kutoka kwa Anas, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, "kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume, rehema na amani zimshukie, kuhusu Saa, akasema: Saa itakuwa lini? Akasema: Umejiandaa vipi kwa ajili yake? Akasema: Sijajiandaa na chochote, isipokuwa ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, akasema: Utakuwa pamoja na unaowapenda. Anas akasema: Hatukufurahi na kitu kama tulivyofurahi na kauli ya Mtume, rehema na amani zimshukie: "Utakuwa pamoja na unaowapenda". Anas akasema: Ninampenda Mtume, rehema na amani zimshukie, na Abu Bakr na Omar na ninatumai kuwa pamoja nao kwa kuwapenda, hata kama sitafanya kama vitendo vyao".
Na miongoni mwa hizo: kutoka kwa Anas kwamba Mtume, rehema na amani zimshukie, amesema: "Mambo matatu yeyote yule atakayekuwa nayo, atapata utamu wa Imani: Anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuliko chochote kingine, na kumpenda mtu, ampende kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na achukie kurudi katika ukafiri kama anavyochukia kutupwa motoni". Na miongoni mwa hizo: kutoka kwa Anas amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, amesema: "Hatamini mja mpaka niwe ninampenda zaidi kuliko familia yake, mali yake, na watu wote".
Na miongoni mwa hizo pia: kutoka kwa Anas, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, amesema: "Siku ya Uhud ilipofika, watu walikimbia kutoka kwa Mtume, rehema na amani zimshukie, na Abu Talha alikuwa mbele ya Mtume, rehema na amani zimshukie, akimlinda kwa ngao yake, na Abu Talha alikuwa mtu wa kurusha mishale, mwenye nguvu, alivunja pinde mbili au tatu siku hiyo, na mtu alikuwa anapita, akiwa na mfuko wa mishale, akisema: Imwage kwa Abu Talha. Mtume, rehema na amani zimshukie, akainua kichwa chake akawaangalia watu, Abu Talha akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, baba yangu na mama yangu wakomboe, usinyanyue kichwa chako usije ukapatwa na mshale kutoka kwa mishale ya watu, shingo yangu iwe badala ya shingo yako!".
Na miongoni mwa hizo pia: kutoka kwa Qais amesema: "Niliona mkono wa Talha umepooza, alimlinda Mtume, rehema na amani zimshukie, siku ya Uhud".
Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, walikuwa wanajitahidi kutekeleza wajibu huu, ambao ni kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na walikuwa wanashindana katika kupata heshima hii, kwa tamaa ya kuwa miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanawapenda.
Jifaneni nao ikiwa hamko kama wao Hakika kujifananisha na watu wema ni mafanikio
Wasikilizaji wangu wapenzi: wasikilizaji wa redio ya Ofisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir:
Tunatosheka na kiasi hiki katika kipindi hichi, ili tukamilishe tafakari zetu katika vipindi vijavyo, InshaAllah Taala, mpaka wakati huo na mpaka tutakapokutana nanyi, tunawaacha katika uangalizi wa Mwenyezi Mungu na hifadhi yake na amani yake. Tunawashukuru kwa usikilizaji wenu mzuri na Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh.